https://play.google.com/store/apps/details?id=com.blog.ya.watanzania


.

.

.
  • Latest News

    .

    Siku Za Mwisho Za Uhai Wa Samuel Doe

    Secretary of Defense Caspar W. Weinberger hosts Armed Forces Full Honors Arrival Ceremony for His Excellency, Commander in Chief Samuel Kanyon Doe, Head of State of the Republic of Liberia outside the Pentagon's River entrance.Rais Samuel Doe katika moja ya ziara zake akiwa rais.
    Alfajiri ya Aprili 12, 1980, kikundi kidogo cha wanajeshi 17 kilijipenyeza ndani ya makazi ya rais , Ikulu jijini Monrovia kikiwa na silaha za kivita mikononi mwao. Walimkuta Rais William Tolbert bado amelala wakamuamsha na kumuua kwa kumpiga risasi na kuhitimisha utawala wake.
    Aliyeongoza kikundi hicho alikuwa askari kijana na wa cheo cha chini, Sajenti Samuel Kanyon Doe, wakati huo akiwa na umri wa miaka 29 tu. Ndiye aliongoza mapinduzi na hatimaye mauaji ya Rais William Tolbert.
    Na inasemwa kuwa Doe alipoingia Ikulu na wenzake, alidhani watakwenda kumlalamikia Rais juu ya mishahara midogo ya askari wa vyeo vya chini. Lakini jinsi walivyoikuta Ikulu ikiwa nyepesi vile, ndivyo mipango ilipobadilika na kuamua kumuua rais mwenyewe na kuchukua madaraka.
    Samuel Doe alikuwa askari ambaye hata madarasa manne ya shule ya msingi hakuyamaliza. Alitoka kabila dogo la waishio misituni, kabila la Krahn. Ni watu wa kabila masikini ambao ndiyo waliotoka vijijini na kukimbilia jijini Monrovia kutafuta vibarua na pesa. Kwa wenye bahati, kama Samuel Doe, walionekana mitaani na kuitwa kujiunga na Jeshi.
    Na kama ilivyokuwa kwa Idi Amin, Urais ulimdondokea tu Samuel Doe, kama vile mtu aliyeshinda bahati nasibu. Ujio wa Samuel Doe uliwafanya Waliberia waamini kuwepo kwa mabadiliko baada ya Kuondoka kwa utawala wa kifisadi na kirasimu wa William Tolbert.
    Samuel Doe akajitangaza kuwa Rais, April 12, 1980. Haraka sana akawatwanga risasi mawaziri wote wa Tollbert, alifanya hayo kwenye pwani ya bahari jijini Monrovia huku wananchi wakitazama kama mechi ya mpira.
    cabinet-ministers-lined-up-for-execution-after-a-coup-detat-in-liberia-1980-2Miili ya mawaziri ikiwa chini baada ya kupigwa risasi hadharani.
    Sajenti Samuel Doe akatawala kwa kipindi cha miaka kumi, nchi ikawa kama imesimama. Watu wa kabila la Samuel Doe waliogopewa na makabila mengine, waliweza kufanya lolote lile na hakuna aliyewagusa, waliua na waliwatisha wengine.Wengi wasio wa kabila la Rais Doe, waliishi kwa hofu kubwa.
    Na kile ambacho kila mtu asiye wa kabila la Doe, alikuwa anakisubiri, ni kushuhudia mwisho wa Sajenti Samuel Doe. Na hapa akatokea Charles Taylor, huyu alikuwa rafiki wa zamani wa Sajenti Samuel Doe. Lakini, urafiki wao ulikufa pale Samuel Doe alipodai kuwa Charles Taylor alimtapeli dola milioni moja, kisha Taylor akatorokea Marekani.
    Huko akaanza kufanya biashara kwa mtaji wa fedha alizomtapeli Sajenti Samuel Doe. Charles Taylor naye akaishia gerezani nchini Marekani kwa mashtaka ya utapeli. Bahati nzuri kwake alifanikiwa kutoroka jela na kukimbilia nchini Ivory Coast.
    Akiwa Ivory Coast, Charles Taylor akaanza kujipanga kwenda kuuangusha utawala wa Sajenti Samuel Doe, akiwa Ivory Coast, aliandaa kikosi cha wapiganaji 60.
    Kikosi kilikuwa tayari kwa kuingia Monrovia kumwondoa Samuel Doe madarakani mwaka 1989. Wakati huo, wajuzi wa masuala ya kijeshi waliamini kabisa, kuwa Sajenti Samuel Doe angeweza, kirahisi kabisa, kumteketeza kijeshi Charles Taylor na kikosi chake cha watu 60.
    Sajenti Samuel Doe angeweza kufanya hivyo hata kabla Charles Taylor hajavikaribia viunga vya Monrovia yalipo makazi ya rais ‘President Palace.’
    Badala yake, ‘Master Sergeant’ Samuel Doe, aliwatuma mstari wa mbele, wanajeshi kutoka kabila lake la Krahn. Ni wanajeshi wa kuokoteza ambao wengine hawakuwa hata na viatu.
    Wanajeshi wale wa Samuel Doe, njiani wakitokea mji mkuu Monrovia wakielekea uwanja wa mapambano, wakaanza kufanya wizi wa pesa, kuiba mali za watu, ubakaji na vitisho dhidi ya raia.
    Habari za askari ‘vibaka’ wa Samuel Doe zikasambaa haraka kwenye vijiji vya msituni nje ya jiji la Monrovia. Huko watu wakajitolea kujiunga na vikosi vya Charles Taylor kukabiliana na askari wa Samuel Doe.
    Jeshi la Taylor likakua kwa haraka, baada ya miezi sita tu, likaingia kwenye viunga vya mji mkuu wa Liberia, Monrovia, June 1990.
    UGOMVI NDANI YA KAMBI YA TAYLOR
    Ndipo hapo kwenye kambi ya Charles Taylor ugomvi ukazuka. Nani atakuwa Rais? Nani atakuwa na mamlaka ya hazina kuu? Ni ugomvi uliowatenganisha Charles Taylor na Prince Johnson aliyekuwa msaidizi wake na Prince aliamua kuachana na Taylor na yeye kuanzisha kikosi chake.
    Wote wawili walikuwa na tamaa ya Ikulu. Vita sasa ikawa ya vikosi vitatu kugombania kuingia Ikulu ya Monrovia; Kikosi cha Sajenti Samuel Doe kinachojihami, kikosi cha Charles Taylor na kikosi cha Prince Johnson.Wote wakaanza kupigana wenyewe kwa wenyewe kugombania Ikulu ya Monrovia.
    Mitaa ya Monrovia wakaonekana askari wa makundi tofauti wakipigana. Hata watoto waliingizwa kwenye vita vile vya kiwendawazimu.
    Hatimaye, mwishoni mwa mwezi Agosti 1990, vikosi kutoka nje viliingilia mgogoro ule, ni vikosi vya Nigeria chini ya mwavuli wa ECOMOG ambao ni umoja wa mataifa ya Afrika magharibi.
    doe8Sajenti Doe akipata maelekezo ya kijeshi.
    Ecomog walikuwa na jeshi lilioongozwa na kamanda kutoka Nigeria. Jeshi hilo lilifika Monrovia na meli kubwa ya kijeshi.
    Jumapili Septemba 9, 1990, Rais Samuel Doe aliposikia habari za ujio wa ECOMOG, akafanya kosa kubwa la kuamua kutoka Ikulu na kwenda mwenyewe bandarini kuonana na kamanda wa vikosi hivyo vya majeshi ya ECOMOG.
    Samuel Doe hakuwa na msafara mkubwa, aliwachukua walinzi wake na kuingia kwenye Mercedes Benz kuelekea bandarini. Maskini! Rais wa nchi akajikuta anapita kwenye mji wenye miba.
    Akafika bandarini na hapo Prince Johnson alikuwa amewapanga askari wake kumshughulikia Samuel Doe, zikapigwa risasi na walinzi wote wa Samuel Doe wakapoteza maisha.
    Samuel Doe mwenyewe risasi ilimpata mguuni na hakuweza kukimbia, akakamatwa. Akafungwa kitambaa usoni na akapelekwa kwenye kuteswa nje kidogo ya jiji la Monrovia. Prince Johnson akahakikisha mateso yale yanarekodiwa kwa kamera za filamu.
    Kwenye filamu hiyo, Prince Johnson anaonekana akipungiwa upepo na mwanadada huku akinywa bia na kumwangalia rafiki yake wa zamani, Samuel Doe akiteswa. Muda mwingi Prince Johnson alikuwa akimtaka Samuel Doe aseme zilipo fedha kwenye hazina.
    Kuna wakati alisikika Samuel Doe akimwita rafiki yake wa zamani kwa jina alilozoea kumwita: “Prince, waambie walegeze kamba walizonifunga, nitasema kila kitu, walegeze hizo kamba kwanza!”
    Ukweli, kamba walizomfunga kwenye miguu na mikono zilikaza sana na kumletea maumivu makali. Waliendelea kumpiga huku wakimtaka ataje ilipo hazina. Walimtaka ataje akaunti yake ya benki.
    Ndivyo ilivyokuwa barani kwetu Afrika, na labda mpaka leo pale rais dikteta anapopinduliwa, kikubwa kinachotafutwa ni namba ya akaunti ya benki alikoficha fedha, mara nyingi ni kwenye benki za nje kisha hufuata hazina ya ndani ya nchi.
    September 1990, Monrovia, Liberia --- Liberian president Samuel Doe is tortured at the hands of the militant group Independent National Patriotic Front of Liberia (INPFL). Responding to years of government corruption and oppression, in 1989 the National Patriotic Front of Liberia (NPFL) launched a revolt against President Doe, seizing control of much of Liberia and plunging the country into massive civil war. During the war Prince Yormie Johnson split from the NPFL and formed the INPFL; then he and his forces captured, tortured, and executed President Doe, recording the gruesome deed on video tape. --- Image by © Patrick Robert/Sygma/CorbisSajenti Samuel Doe akiwa mikononi mwa wanajeshi watiifu wa Prince Johnson
    “Mkateni sikio kama hataki kusema!” Alisikika Prince Johnson akitamka kwa hasira baada ya Doe kugoma kutaja mahali alikoficha fedha wala kutaja namba ya akaunti.
    Askari wale wakamtupa Samuel Doe sakafuni, wakamkata sikio moja.
    “Mkateni sikio lingine!” Alisikika tena Prince Johnson akitamka. Baada ya hapo, Rais Doe aliuawa kikatili Jumapili hiyo jioni, Septemba 9, 1990 baada ya kukatwa masikio yake, sehemu zake za siri na baadhi ya vidole vya miguu na mikono na hatimaye mwili wake ulitembezwa mitaa mbalimbali ya jiji la Monrovia.
    September 1990, Liberia --- Liberian soldiers pose with their rifles around the displayed dead body of President Samuel Doe during the Liberian Civil War. Prince Yormie Johnson, leader of the Independent National Patriotic Front of Liberia (INPFL), tortured and murdered Doe after his capture by peacekeeping forces. Doe's ears and fingers were cut off on camera during the attack. --- Image by © Patrick Robert/Sygma/CorbisMwili wa Samuel Doe ukitembezwa mitaani baada ya kuuawa.
    Huo ndio ulikuwa mwisho wa Dikteta Samuel Kanyon Doe wa Liberia. Kifo chake kiliacha nyuma makundi mawili hasimu moja likiongozwa na Prince ambalo lilifanikiwa kumuaa dikteta Samuel Doe na lingine likiongozwa na Charles Taylor.
    Je? Nani alifanikiwa kuwa rais wa Liberia baada ya mauaji hayo? Hazina ilimilikiwa na nani? Samuel Doe alitaja kiasi cha pesa alichokificha nje ya Liberia?
    https://play.google.com/store/apps/details?id=com.blog.ya.watanzania

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Post a Comment

    Item Reviewed: Siku Za Mwisho Za Uhai Wa Samuel Doe Rating: 5 Reviewed By: news
    Scroll to Top