WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amepokea jumla ya sh. bilioni 1.040 kutoka kwa
watumishi na wadau mbalimbali zikiwa ni misaada kwa wananchi
walioathirika na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera Septemba
10, mwaka huu.
Makabidhiano
ya michango hiyo, yamefanyika leo mchana (Jumanne, Septemba 20, 2016)
kwenye ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam.
Akikabidhi
hundi kwa Waziri Mkuu, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi alisema
kiasi cha sh. 1,000,030,100 kimekusanywa kutoka kwa watumishi wa idara
na Wizara zote za Serikali na kwamba michango zaidi bado inaendelea
kukusanywa.
“Tunaamini
michango hii itasaidia kuwafuta machozi wenzetu waliopatwa na maafa
japokuwa tunajua haitatosha kurudisha kile walichopoteza. Tuna imani
itasaidia kupunguza makali ya machungu waliyoyapata,” amesema.
Hata
hicyo, Balozi Kijazi amemhakikishia Waziri Mkuu kwamba bado wanaendelea
kukusanya michango kutoka kwenye nyingine ambazo zilichelewa kupata
taarifa na kwamba wakikamilisha wataiwasilisha mapema iwezekanavyo.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amepokea michango ya sh. milioni 40 na kati
ya hizo, sh. milioni 20 zimetolewa na kampuni ya ujenzi ya CHICO ya
China na sh. milioni 20 nyingine zimetoka kwa Umoja wa Wafanyabiashara
na Wenye Viwanda wa India waliopo nchini (India Business Forum).
Akiwasilisha
mchango wake, Mwakilishi Mkuu wa kampuni ya CHICO hapa nchini, Bw. Guo
Zhijian alisema wamesikitishwa na maafa yaliyotokea mkoani Kagera.
“Tumefanya miradi mingi mkoani Kagera ikiwemo ujenzi wa barabara za
urefu kilometa 300, kwa hiyo mkoa huu tunaujua zaidi. Tunatoa pole kwa
wote waliopatwa na maafa hayo,” amesema.
Naye
Mwenyekiti wa umoja wa wafanyabiashara na wenye viwanda kutoka India
(IBF), Bw. Gagan Gupta alimweleza Waziri Mkuu kwamba wameshtushwa na
tukio hilo na kwamba wametanguliza kiasi hicho ili kisaidie juhudi za
Serikali katika kukabiliana na maafa hayo.
“Bado tunaendelea kuwasiliana na wenzetu wengine na tukipata michango zaidi tutaiwasilisha mapema iwezekanavyo,” amesema.
Akitoa
shukrani kwa waliotoa michango yote hiyo, Waziri Mkuu amewashukuru kwa
misaada hiyo na kuahidi kuwa Serikali itahakikisha michango hiyo
inafikishwa Kagera kwa walengwa.
“Tunashukuru
sana kwa michango yote. Michango hii ni muhimu na inaonyesha mshikamano
wa dhati uliopo. Michango hii inaonyesha kuguswa na mapenzi ya dhati
kwa waliopatwa na maafa. Napenda niwahakikishie kuwa Kamati za Maafa za
Mkoa, Ofisi ya Waziri Mkuu na kamati za wilaya, ziko pale kuhakikisha
walengwa wanafikiwa,” ameongeza.
Waziri
Mkuu amesema Serikali inakamilisha tathmini ya maafa hayo na kuahidi
kutoa taarifa ya kiasi kilichokusanywa na kiasi kilichotumika. Amewaomba
wananchi waliotoa ahadi zao za michango wakamilishe ahadi zao.
“Ninawaomba
wale walioahidi kutoa michango wakamilishe ahadi zao na wale walio
mbali na benki watumie namba za simu zilizotolewa mahsusi kwa ajili ya
kuchangia maafa hayo,” amesisitiza.
Akaunti
ya maafa imefunguliwa katika Benki ya CRDB yenye namba 015 222 561 7300
kwa jina la KAMATI MAAFA KAGERA – Swiftcode: CORUtztz na namba za simu
za mkononi zinazotumika kupokea michango hiyo ni 0768-196-669 (M-Pesa)
au 0682-950-009 (Airtel Money) au 0718-069-616 (Tigo Pesa).
Tetemeko
hilo lililotokea Jumamosi, Septemba 10, mwaka huu, lilisababisha vifo
vya watu 17 na wengine 440 kujeruhiwa. Kati yao, watu 253 walifikishwa
Hospitali ya Mkoa, 153 walilazwa, 113 walitibiwa na kuruhusiwa na
wengine 38 wanaendelea na matibabu ambapo kati yao watu 23 wamefanyiwa
upasuaji mkubwa na wanaendelea vizuri.
Pia
tetemeko hilo limesababisha nyumba 2,063 kuanguka huku nyingine 14,081
zikiwa katika hali hatarishi baada ya kupata nyufa na 9,471 zimepata
uharibifu mdogo huku wananchi 126,315 wakihitaji misaada mbalimbali.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 - DAR ES SALAAM.
JUMANNE, SEPTEMBA 20, 2016.
0 comments:
Post a Comment