TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Waziri Mahiga apokea Dola elf 50,000 kwa ajili ya Waathirika wa Kagera
Serikali
ya Jamhuri ya Korea imetoa msaada wa Dola za Marekani elf 50,000
takribani milioni 108 kwa fedha za Tanzania kwa ajili ya waathirika wa
tetemeko la ardhi lilitokea mkoani Kagera mwezi Septemba 2016.
Msaada
huo ulikabidhiwa leo jijini Dar es Salaam na Balozi wa Korea nchini
Tanzania, Mhe. Song Geum Young na kupokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga (Mb) kwa niaba
ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa
(Mb).
Baada
ya kupokea msaada huo, Dkt. Mahiga aliishukuru Serikali ya Korea na
kuahidi kuwa msaada huo ataukabidhi kwa Mhe. Waziri Mkuu ili uweze
kutumika kama ulivyokusudiwa.
Mhe.
Mahiga alisema kuwa Korea imekuwa mbia mkubwa wa Tanzania tokea nchi
hiyo ilipoanzisha mahusiano ya kidiplomasia na Tanznaia miaka 25
iliyopita. Alieleza kuwa katika kipindi hicho Tanzania imekuwa ikipokea
misaada mbalimbali ya kiuchumi, kijamii na ya kibinadamu ukiwemo huu wa
leo ulioelekezwa kwa waathirika wa tetemeko la ardhi la mkoani Kagera.
Mhe.
Waziri alitaja misaada ambayo Korea imeipatia Tanzania ni pamoja na
ujenzi wa daraja la Malagarasi mkoani Kigoma, ujenzi wa hospitali ya
kisasa ya Mloganzila na ujenzi wa hospitali ya uchunguzi wa afya ya Mama
iliyopo Chanika. Aidha, Korea hivi karibuni itaanza ujenzi wa daraja la
Selander ambalo linatarajiwa kuanzia ufukwe wa Coco, Oysterbay hadi maeneo ya hospitali ya Aga Khan, Upanga jijini Dar es Salaam.
Waziri
Mahiga alibainisha pia kuwa Jamhuri ya Korea itatoa msaada mkubwa
zaidi wa maendeleo kwa Tanzania kuliko nchi yeyote ya Afrika. Taarifa
hiyo ilitolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea, Mhe. Yun Byung-se
alipofanya naye mazungumzo kando ya Mkutano wa nchi za Afrika na
Korea uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia tarehe 06 na 07 Desemba 2016.
Kwa
upande wake, Balozi wa Korea nchini aliahidi kuwa nchi yake itaendelea
kushirikiana na Tanzania hususan kutoa atia misaada ya maendeleo ili
iweze kutimiza azima ya Serikali ya awamu ya tano ya kuifanya Tanzania
kuwa nchi ya viwanda.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 27 Desemba 2016.
|
0 comments:
Post a Comment