WAZIRI
Mkuu Kassim Majaliwa atamtuma mara moja Msajili wa Hazina, aende kufanya
uchunguzi wa kina na wa kijinai (forensic investigation) ili
kijiridhisha kama mapato na matumizi ya kampuni ya TANCOAL ni
halali.Alitoa kauli hiyo jana mara baada ya kupokea taarifa na
kutembelea mgodi huo ili kuona shughuli za uzalishaji zikoje.Waziri Mkuu
alisema atamuagiza pia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu ya Serikali
(CAG) ili apitie mahesabu ya kampuni hiyo tangu mwaka 2011 walipoanza
uzalishaji.
“Mbali na
CAG, itabidi Gavana wa Benki Kuu naye aangalie utumaji wa fedha
uliokuwa ukifanywa kama ulifanyika kwa halali,” alisema.
Katika
maswali aliyoyauliza Waziri Mkuu, alitaka kufahamu ni kwa nini kampuni
hiyo haijalipa gawio kwa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) ambao ni
mbia (asilimia 30) na kampuni ya Intra Energy Limited (asilimia 70),
licha ya kuwa imekuwa ikifanya uzalishaji wa makaa ya mawe na
kuyasafirisha kwenye viwanda hapa nchini na nje ya nchi.
“Taarifa
zenu zinaonyesha kuwa mmepata kila mwaka, lakini rekodi nilizonazo
zinanionyesha kuwa mwaka 2013 mlipanga kuzalisha tani 50,000 na mkauza
zaidi ya hapo. Mkaguzi wa Hesabu anasema kampuni imepata, hii
itawezekanaje?” alisema wakati akimhoji Mkurugenzi Mtendaji wa NDC,
Mlingi Mkucha.
“Desemba
2013 mliuza tani 39,000 kwa wamiliki wa viwanda vya nguo, pia mliuza
tani 2,000 kwa Kampuni ya Saruji ya Zambia, Novemba 2013 mliingia
makubaliano ya kuuza tani 165,000 kwa kampuni ya saruji ya Tanzania na
ziliuzwa. Mbona ‘financial statement’ zenu zinasema mwaka huo nao
mlipata hasara?” “Mnasema gawio (dividend) hutolewa baada ya mtu
kutangaza faida. Mbona mlivuka lengo lakini mkatangaza kuwa kampuni
imepata hasara katika mwaka huo wa fedha?” alihoji Waziri Mkuu.
Waziri
Mkuu alimbana Mkucha aeleze ni kwa nini akiwa mwanasheria wa NDC,
aliruhusu kuwepo kwa mkataba unaotoa mwanya kwa kampuni ya TANCOAL
kulipia gharama za menejimenti kwa wakurugenzi ambao wako Australia,
wakati hawahusiki na utendaji wa kila siku wa TANCOAL hapa nchini.
Alihoji
pia kwa nini aliyekuwa Mkurugenzi wa NDC, Gideon Nassari alikuwa ni
mjumbe wa Bodi ya TANCOAL na mjumbe wa Bodi ya Intra Energy Corporation
ya Australia huku akiwa ni Mtendaji Mkuu wa NDC.
“Wewe
ulikuwa mwanasheria wa NDC na ulilijua hilo, lakini hukuona taabu ya
kiutendaji katika hilo? Au ulishindwa kusema kwa sababu alikuwa ni bosi
wako?” Waziri Mkuu alihoji.
Alimtaka
Mkucha apeleke mkataba huo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili aupitie
upya, na hasa kipengele cha kufungua akaunti za NDC kwa kutumia kanuni
za Australia na suala la utaratibu wa gawio kwa wanahisa, ambapo kifungu
kilichopo kinaipa Bodi ya TANCOAL mamlaka ya kuamua kutoa au kutokutoa
kwa wanahisa.
“Kipengele
kama hiki kwenye mikataba kinazuia ninyi kupata gawio, na ndiyo maana
hesabu za kila mwaka zimekuwa zinasoma hasara na ninyi mnaona sawa tu
huku Serikali ikiendelea kukosa mapato yake,” alisema.
Waziri
Mkuu aliutaka uongozi wa kampuni ya TANCOAL, uongeze uzalishaji ili
uweze kukidhi mahitaji ya ndani, kwani makampuni mengi yamebaini gharama
kubwa iliyopo kwenye matumizi ya mafuta ya dizeli na sasa yanahitaji
makaa ya mawe kwa uzalishaji.
“Nimetembelea
mgodi na kujiridhisha kuwa makaa ya mawe yapo ya kutosha. Uongozi wa
kampuni mmesema mashine ziko bandarini Mtwara, lipieni mkamilishe
taratibu ili mashine na mitambo yenu vije kusaidia kuongeza uzalishaji,”
alisema.
Waziri
Mkuu alisisitiza kuwa serikali haitaruhusu uagizaji wa makaa ya mawe
kutoka nje ya nchi na kwa maana nyingine, imeongeza wigo wa soko.
Lakini, alisema anaona wanakosa teknolojia uchimbaji makaa kwa wingi na
kuwataka wafanye haraka kuleta vifaa hivyo vilivyoko bandarini.
0 comments:
Post a Comment