Mbwana Samatta kulia akiwa na Jamal Bakhresa na Thomas Ulimwengu kushoto jana mjini Lubumbashi
MSHAMBULIAJI Mbwana Ally Samatta amerejea jana mjini Lubumbashi
kuendelea na maisha chini ya utawala wa Moise Katumbi Chapwe, rais wa
klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Samatta akiwa na Mtanzania mwenzake anayecheza naye Mazembe, Thomas
Ulimwengu wamepiga picha na mmoja wa Wakurugenzi wa klabu ya Azam FC ya
Dar es Salaam iliyo ziarani Lubumbashi, Jamal Bakhresa.
Na jamal Bakhresa ameituma picha hiyo BIN ZUBEIRY jana akisema amefurahi kukutana na vijana na kuzungumza nao mawili matatu.
Habari zaidi kutoka Lubumbashi zinasema kwamba, klabu ya CSKA Moscow
ya Urusi iliamua kuachana na Samatta kwa sasa baada ya kuumia enka akiwa
katika wiki ya kwanza ya majaribio.
Kiongozi mmoja wa Mazembe ambaye hakupenda kutajwa jina, ameiambia
BIN ZUBEIRY jana usiku kwamba timu hiyo ya Ulaya ilivutiwa na uwezo wa
mshambuliaji huyo wa Tanzania, lakini ilishindwa kumtathmini zaidi baada
ya kuumia.
Hata hivyo, amesema klabu (TP Mazembe) chini ya Rais, Moise Katumbi
bado wapo bega kwa bega kuhakikisha wanatimiza ndoto za mtoto wa
Mbagala, Samatta kucheza Ulaya kwa maslahi makubwa.
Mapema mwezi huu, Samatta alipata fursa ya kufanya mazoezi na klabu
ya CSKA Moscow ya Urusi ambayo ilikuwa inamjaribu kwa ajili ya kumnunua,
hata hivyo bahati mbaya kwake aliumia enka.
Samatta ambaye amebakiza mwaka mmoja katika Mkataba wake TP Mazembe
tangu asajiliwe kutoka Simba SC ya Dar es Salaam, alipania mno Januari
hii kuhamia Ulaya, lakini inaonekana wakati wake bado.