Mpira wa Pete, New Habari Waogelea Magoli 46-2
MASHINDANO
ya NSSF Media Cup yameendelea kupamba moto ambapo timu ya mpira wa
miguu ya NSSF imeichalaza bila huruma timu ya Jambo Leo kwa magoli 3 kwa
mtungi. Mchezo huo mkali ambao uliwafanya wachezaji wa timu ya Jambo
Leo kukimbia uwanjani kutokana na mvua ya magoli mfululizo ulivunjika
dakika ya 69.
Mwamuzi
wa mpambano huo alilazimika kumaliza mchezo baada ya kuwasubiri
wachezaji wa Jambo Leo kurudi uwanjani kwa dakika 15 bila ya mafanikio
kisha kuamua kumaliza pambano na kutoa ushindi kwa timu ya NSSF. Hadi
pambano hilo linasimama katika dakika ya 69 NSSF ilikuwa ikiongoza kwa
magoli 3 kwa mtungi.
Wachezaji
wa Jambo Leo walitoka uwanjani kwa kudai hawawezi kumalizia mchezo huo
kutokana na hali ya uwanja ambapo ulikuwa umejaa madimbwi ya maji kwa
baadhi ya maeneo kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar es
Salaam.
Jambo
Leo waliomba pambano hilo lisimamishwe na kuendelea kesho au siku
nyingine ambapo uwanja ulikuwa katika hali nzuri tofauti na ilivyokuwa.
Hata
hivyo Kamisaa wa Mchezo huo, Majuto Omary alisema mpambano huo hauwezi
kurudiwa maana kanuni za mashindano haziruhusu na kuongeza kuwa kama
Jambo Leo waliona uwanja ni mbovu wangeligoma tangu awali na sio
kusubiri mchezo uchezwe hadi dakika ya 69.
"...Kanuni
za mashindano haya haziruhusu wanachotaka Jambo Leo, kwanini wakimbie
uwanjani baada ya kufungwa magoli matatu...mbona hawakugoma tangu mchezo
haujachezwa hii ni janja yao wameona wamefungwa tena magoli mengi ndio
wakimbie uwanja hii haikubaliki, ushindi utaenda kwa aliyeshinda na
pambano halirudiwi," alisema Omary.
Mvua
ya magoli nyingine katika mashindano hayo iliwakumba timu ya Mpira wa
Pete wasichana ya New Habari ambapo ilichalazwa magoli 46 kwa mawili na
timu ya Business Times wasichana katika mchezo wao uliofanyika TTC
Chang'ombe. Katika mchezo huo Business Timu walionekana kuutawala mchezo
kwa muda wote na kuwapeleka puta akinadada wa New Habari kabla ya
kuogelea mvua hiyo ya magoli.
Katika
mchezo mwingine wa mpira wa miguu, Timu ya Uhuru Media iliichapa Sahara
Media kwa magoli 2-1. Timu ya Sahara ndio waliokuwa wa kwanza kupata
goli ambapo walipachika bao la kwanza katika dakika 26 kupitia kwa
mchezaji wao Deodatus Nkwabi alilofunga kwa kichwa.
Uhuru walikuja juu dakika 46 ambapo mchezaji wao Mussa Gadi alifunga
goli kwa mpira wa adhabu na kusawazisha mchezo. Mchezaji wa Uhuru Media,
Ayub Malale alicheka na nyavu za Sahara Media katika dakika 87 baada ya
kuunganisha crosi na kufanikiwa kufunga bao la pili. Hadi mwisho wa
mchezo huo Uhuru 2 na Sahara 1.
Mashindano
ya NSSF Media cup yanaendelea katika viwanja vya TCC Chang’ombe na
Bandari Jijini Dar es Salaam, yakihusisha mpira wa miguu na mpira wa
Pete ambapo vyombo mbalimbali vya Habari vinashiriki michezo hiyo.
Mashindano hayo yanaambatana na wiki ya Huduma Kwa wateja ya NSSF ambapo
wateja watapata fursa ya kupata elimu kuhusu huduma za NSSF.
Kama
wewe ni Mkazi wa Dar es Salaam Tafadhali tembelea banda la NSSF katika
viwanja vya TCC Chang’ombe kuanzia Tarehe 20/03/2015 hadi Tarehe
29/03/2015 saa 03:00 asubuhi hadi 11:00 jioni.
Mwanachama
ataweza kupata taarifa ya michango yake, Kujiandikisha Kwa Wanachama
wapya na vile vile watapata elimu kuhusu huduma mbalimbali za NSSF.

