Na. Sylvester Onesmo wa Jeshi la Polisi Dodoma.
Jeshi
la Polisi Mkoa wa Dodoma linawashikilia watu sita (6) kwa makosa
mbalimbali yakiwemo ya kumiliki silaha kinyume cha sheria, kulima na
kukutwa na bhangi pamoja na kuingia nchini bila kibali, kufuatia
operesheni inayoendelea Mkoani Dodoma kusaka watuwanaojihusisha na
uhalifu wa aina mbalimbali.
Akithibitisha
matukio hayo kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi
Mwandamizi wa Polisi DAVID MISIME - SACP amewataja watu wanaoshikiliwa
na Polisi kuwa ni ERASTO DIHELELA mwenye miaka 31, mkulima, mkazi wa
kijiji cha Lukole aliyekamatwa na silaha aina ya Gobore isiyokuwa na
namba pamoja na Golori zake 11 na vipande 17 vya nondo akilimiliki bila
kuwa na kibali. Mtuhumiwa huyo pia alikutwa amelima bhangi kwa
kuchanganya na mahindi katika shamba lake la hekari moja.
Mtu wa
pili ni HAPPY GIBSON mwenye miaka 28, mkulima, mkazi wa Kijiji cha
Lukole akiwa na silaha aina ya Gobole nyumbani kwake bila kuwa na kibali
cha kumiliki silaha hiyo. Vile vile katika kupekuliwa nyumbani kwake
mtuhumiwa huyu alikutwa na bhangi kilo tano (5) alizohifadhi ndani ya
nyumba yake tayari kwa kusafirisha.
Kamanda
MISIME amesema katika oparesheni hiyo pia amekamatwa HAMISI MWIKOLA
mwenye miaka 28, mkulima, mkazi wa Kijiji cha Lukole akiwa amelima
bhangi kwa kuchanganya ndani ya shamba lake la mahindi hekari mbili.
Watuhumiwa
hawa wote wamekamatwa siku ya tarehe 21/03/2015 katika kitongoji cha
shuleni mlimani kijiji cha Lukole kata ya Kingiti tarafa ya Kibakwe
Wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma na watafikishwa mahakamani mara baada ya
taratibu kukamilika.
Aidha
Kamanda MISIME amesema wamekamatwa raia wawili kutoka Ethiopia katika
eneo la Nala Dodoma Mjini wakiwa hawana kibali cha kuingia nchini na
kuishi. Watu hao ni GETHGACHEW ANCHISO mwenye miaka 29, na KONJITI FEYSA
mwenye miaka 23.
Vilevile
huko katika kijiji cha Tubugwe juu kata ya Chamkoloma Tarafa ya Mlali
Wilayani Kongwa amekamatwa mtu mmoja anayefahamika kwa jina la MWAJABU
SALUM mwenye miaka 28, mkulima, mkazi wa Tubugwe juu akiwa amelima
bhangi ndani ya shamba lake la mahindi la hekari mbili na nusu (2 ½).
Kamanda
MISIME ametoa wito kwa wakulima kutolima mazao haramu na badala yake
walime mazao yenye tija kwa maendeleo halali kwani hatima ya wahalifu
wanaolima bhangi na kukutwa na silaha bila kibali ni kuishia jela na
kuzitesa familia zao kwa vitendo wanavyofanya vya kihalifu. Aidha
amewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi
kuwafichua watu wanaomiliki silaha kinyume cha sheria, kulima na
kumiliki au kuuza dawa za kulevya na kujihusisha vitendo vingine vya
kihalifu katika maeneo yote ya Mkoa wa Dodoma kwa usalama wa wananchi
kwa ujumla na kutokomeza uhalifu wa aina zote.
Watuhumiwa waliokuwa wakilima Bhangi hiyo.




