HALMASHAURI ya Manispaa ya Ilala imeendesha harambee ya uchangiaji wa madawati kwa shule zake za msingi 113.
Akizungumza
katika hafla ya uchangiaji wa madawati hayo iliyopewa jina la ‘Usiku wa
Mswahili’ Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi alisema Halmashauri
hiyo inakabiliwa na uhaba wa madawati yapatayo12,000.
“Halmashauri
yetu ina wanafunzi takriban 150,800 ambapo wanafunzi walioandikishwa
darasa la kwanza kwa mwaka huu ni 22,000, baada ya kufanya tathmini
tukagundua shule zetu zina uhaba wa madawati ndipo tukakubaliana kufanya
harambee hii,” alisema.
Alisema wadau mbalimbali wa elimu nchini wameitikia wito huo na kwamba tayari wamepata kupata kiasi cha madawati 1,173.
“Hii
inatia moyo kwamba tunaweza kumaliza changamoto hii tuliyonayo, hivyo
nitoe wito kwa jamii kubadili mtazamo wao na kuanza kuchangia shughuli
za kimaendeleo zenye tija kwa Taifa kama elimu na afya, hapa tunajenga
rasilimali watu ambao watakuja kulitumikia Taifa katika siku zijazo,” alisema.
Kwa
upande wake Ofisa Elimu Idara ya Elimu ya Msingi wilayani humo,
Elizabeth Tomas alisema mbali na changamoto hiyo ya uhaba wa madawati
pia wanakabiliwa na uhaba wa madarasa.
“Tulitafakari…
kwanini wanafunzi wanamaliza wakiwa na tatizo la mwandiko mbaya huku
wengine wakiwa hawajui kusoma na kuandika tukagundua tatizo ni ukosefu
wa madawati hasa kwa wale wanaoingia darasa la kwanza.
“Hawa
hulazimika kusomea yale ya wakubwa kwa maana hiyo tumejipanga
kutengeneza ya kimo chao takriban madawati 5,231, tukimaliza hilo
tutageukia upande wa madarasa,” alisema.


