https://play.google.com/store/apps/details?id=com.blog.ya.watanzania


.

.

.
  • Latest News

    .

    Ahadi za watangazania CCM ni unafiki, uongo au wameokoka?

    Hadi sasa wanachama 38 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamechukua fomu kuomba uteuzi wa kupeperusha bendera ya chama hicho tawala katika nafasi ya urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka huu.
    Miongoni mwa watangazania hao, wamo viongozi wa watendaji wakuu ndani ya Serikali ya sasa akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk Mohamed Gharib Bilal na Waziri Mkuu, Mizengo Peter Pinda.
    Katika orodha hiyo pia wamo mawaziri wakuu wa zamani wawili, Frederick Sumaye aliyeshikilia wadhifa huo kwa miaka 10 mfululizo wa serikali ya awamu ya tatu chini na Benjamin Mkapa, na Edward Lowassa aliyeshikilia wadhifa huo katika miaka ya mwanzo ya awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete.
    Wamo mawaziri wanaotumikia Serikali ilioko madarakani pamoja na waliowahi kushikilia uongozi wa wizara kadhaa katika awamu mbalimbali za serikali, kuanzia awamu ya tatu na ya nne.
    Kundi hilo pia linajumuisha wabunge kadhaa machachari wa CCM, wasomi, wana diplomasia na wanachama wa kawaida wa chama hicho.
    Wengi wa watangazania hao wamekuwa wakitoa ahadi, misimamo na ilani zao binafsi kuhusu vipaumbele vyao na kero zinazoikabili jamii watakazozivalia njuga iwapo watateuliwa na chama chao kugombea na kushinda urais. Hii ndiyo hoja yangu leo.
    Sitataja vipaumbele na kero zote zinazotajwa na watangazania hao. Bali nitataja chache tu kwa sababu ndizo nimelenga kuzitolea hoja.
    Rushwa, huduma duni kwenye sekta ya elimu, maji, afya, miundombinu na mmomonyoko wa maadili ni kati ya kero zinazotajwa na baadhi ya watangaza nia ndani ya CCM ambao baadhi aidha ni Mawaziri katika Serikali ya sasa au wamewahi kuwa Mawaziri na pengine kushika nyadhifa kubwa zaidi ya uwaziri.
    Mwanzoni nilipata shida sana kuamini maskio yangu kila nilipowasikiliza watangaza nia hawa kwa kujiuliza kwanini wanazungumza maneno na kauli tulizozoea kuzisikia kutoka kwa washindani wao kisiasa.
    Baada ya kujirudi na kukubali kuwa kauli na maneno yao yana ukweli kwa sababu hayo ni baadhi ya kero kubwa katika jamii yetu, mawazo hayo yamenitoka kwa kupata mawazo mapya.
    Hata hivyo nimeijiwa na wazo linguine baada ya kutafakari kwa kina na kurejea michango, kauli na matendo ya baadhi a watangaza nia hao ndani na nje ya bunge pale wenzao kutoka vyama shindani wanapotoa kauli zinazofanana na wanazozitoa hivi sasa.
    Kwa kauli zao wenyewe, watangaza nia hawa wa CCM wanatoa muelekeo kuwa aidha serikali inayoongozwa na chama chao kimeshindwa au viongozi wake, wakiwemo wao hawana uwezo au utashi wa kushughulikia kero hizi.
    Sitaki kuwataja kwa majina kuepuka kuonekana kuwaponda au kuwabeba baadhi ya wagombea. Lakini itoshe tu kusema wapo baadhi ya mawaziri na viongozi wa serikali waliofikia hatua ya kuwabeza na hata kutupa chini ndani ya ukumbi wa bunge hotuba za mawaziri vivuli vilivyokuwa vikiainisha matatizo haya wanayoyataja sasa, na namna ya kuyapatia ufumbuzi.
    Viongozi hawa wanaotaja kero hizi na kujinasibu kuyapatia ufumbuzi wakiukwaa urais walifikia hatua ya kuwaita majina mabaya na ya kejeli wabunge wenzao wa vyama shindani, kila waliposema vitendo vya rushwa na ufisadi vimekithiri nchini na ndani ya serikali yenyewe.
    Kwa jinsi mawaziri hawa walivyokuwa wakijibu kwa ukali na kebehi hoja za wenzao wa vyama shindani kuhusu huduma duni za kielimu, kiafya, maji nimefikia hitimisho kwa kufikiria mambo mawili.
    Mosi, yawezekana viongozi hawa wa serikali na wastaafu wamejitafakari baada ya kuwatukana wenzao wa vyama shindani na kubaini ukweli kwenye hoja zao lakini wakaona aibu kujitokeza hadharani kukiri na kuomba radhi. Yaani ‘wameokoka’ lakini hawataki kutoa ushuhuda.
    Pili, yawezekana viongozi hawa walifanya unafiki walipoamua kuwakebehi na kuwatukana wenzao walipojaribu kuainisha kero na matatizo yanayowakabili wananchi kwa ajili ya kukilinda chama chao na serikali yake.

    Na tatu nafikiria kwamba viongozi hawa ni waongo, hawako tayari na wala hawana nia ya kuyashughulikia matatizo na kero hizi, bali wanayataja kama mtaji wa kisiasa na watarejea kule kule walikokuwa baada ya kuingia madarakani, kubeza wanaotaja kero zinazowakabili wananchi na namna ya kuyatatua. Ikiwa hivyo, basi ile kauli iliyozoeleka ya mbunge wa Iringa mjini, Mchungaji Peter Msigwa kuwa matatizo hayawezi kutatuliwa na watu wale wale walioyaleta/kuyasababisha, kwa mtindo ule ule na mfumo ule ule. Mungu ibariki Tanzania!
    0766 434 354.
    Credit mwananchi
    https://play.google.com/store/apps/details?id=com.blog.ya.watanzania

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: Ahadi za watangazania CCM ni unafiki, uongo au wameokoka? Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top