Iringa/Mwanza/Tabora/Mara. Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa jana alisema kuwa muda wa mabadiliko aliyotabiri Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere ni sasa na kwamba yeye ndiye anayeweza kuyaongoza.
Wakati Lowassa akisema hayo mjini Iringa, kada
mwingine anayewania urais kwa kupitia chama hicho, William Ngeleja
alikuwa mkoani Mwanza ambako alisema kuwa ana dhamira ya dhati na nia ya
kuleta mabadiliko kwa maisha ya Watanzania.
Mjini Iringa, Lowassa alisema kuwa kwa sasa CCM
inahitaji mabadiliko makubwa na akanukuu kauli ya Mwalimu Nyerere
aliyoitoa mwaka 1995 alipozungumzia haja ya chama hicho kujisahihisha.
“Baba wa Taifa alisema kuwa Watanzania wanahitaji
mabadiliko na wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM,”
alisema mbunge huyo wa Monduli kwenye hafla hiyo iliyofanyika Uwanja wa
Samora mjini Iringa.
“Huu ni wakati wa mabadiliko. CCM ikijipanga inaweza kuleta mabadiliko na mtu wa kuleta mabadiliko hayo ni mimi,” alisema.
Lowassa alisema aliamua kuingia kwenye mbio za
urais kwa sababu tatu, ambazo ni kufanya mabadiliko ndani ya CCM,
kufanyia kazi tatizo la umaskini na kushughulikia tatizo la ajira kwa
vijana.
Kwa mujibu wa katibu wa CCM wa Wilaya ya Iringa
Mjini, Zongo Lobe Zongo, jumla ya wanachama 58,562 kutoka wilaya zote
walijitokeza kumdhamini.
Mjini Mwanza, Ngeleja alipata wadhamini 1,253 na kusisitiza hajatumwa na mtu kugombea urais na wala hana kundi.
“Naomba ifahamike kwamba mimi kugombea kwangu
urais sijatumwa na mtu, wala sipo kwenye kundi la mtu yoyote. Naona
natosha na uwezo huo ninao kama Mungu atanijalia kupata nafasi hiyo
nitadhihirisha kwa vitendo,” alisema Ngeleja.
“Mambo niliyoyafanya nikiwa msaidizi wa Rais
Kikwete yanatosha kuonyesha wazi kwamba nina uwezo wa kuboresha mambo
mbalimbali na kukuza uchumi wetu,” alisema ambaye alikuwa Waziri wa
Nishati na Madini.
Ngeleja alirudia kutaja vipaumbele vyake kuwa ni
kudumisha amani na utengamano wa kitaifa, kupiga vita ufisadi, rushwa na
mmomonyoko wa maadili, kuboresha sekta za kilimo, uvuvi, ufugaji,
viwanda, miundombinu na elimu.
Mkoani Mara, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Bernard Membe amesema ni wanaume wachache wa kuigwa kama
Makongoro Nyerere wenye uthubutu wa kusema ukweli kwa uwazi na kwa
kujiamini kuhusu mambo yanayoendelea ndani ya CCM.
Membe alisema hayo alipokwenda Mara ambako alidhaminiwa na wanachama 1,800.
Mbunge huyo wa Jimbo la Mtama alisema Mara ni kati
ya mikoa ya kuenziwa nchini kwa kuwa ndiko anakotoka mwasisi wa Taifa,
na kushauri wagombea wote kuhakikisha wanapita mkoa huo kupata baraka za
kiongozi huyo ambaye aliiacha nchi hii ikiwa na amani na upendo.
Aliwasihi Watanzania wasimchukie mtu pale anaposema ukweli wa mambo kama anavyofanya Makongoro Nyerere.
Alisema Mwalimu Nyerere akifufuka hivi sasa
anaweza kulia kutokana na mambo machafu yanayoendelea ndani ya nchi
ambayo hakuyaacha, kwa kuwa watu wamekuwa waoga kusema ukweli kwa
kuhofia kuchukiwa na wengine.
“Uongozi wa woga unasababisha nchi kuanguka, hivyo
mimi binafsi ninamshukuru Makongoro Nyerere kwa kuwa muwazi, mkweli
bila woga hawa ndiyo wanaume wanaotakiwa tusioneane haya tuelezane
ukweli, kwani Makongoro hata mimi nikikosea huwa ananieleza bila
kumung’unya maneno,” alisema.
January na majawabu mapya
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba alikuwa jijini Mwanza ambako alipata
mapokezi makubwa na kusisitiza kuwa ameamua kuwania urais ili kuwapatia
Watanzania majawabu mapya ya matatizo yao.
Alisema anataka kuwatumikia wananchi na
kuwatatulia changamoto zinazowakabili, likiwamo suala la ukosefu wa
ajira na kuwainua wanawake kiuchumi.
Alirejea kuwaonya watangazania wa CCM kuacha
malumbano na kutukanana majukwaani akisema mwishoni mwa harakati hizo
chama kitakuwa na mgombea mmoja.
“Niwaonye wagombea wenzangu kuwa sioni haja ya
kusimama jukwaani na kuanza kusema fulani yuko hivi wala vile, kikubwa
kuwa na hoja kwa wananchi na namna ya kuwatatulia changamoto
zinazowakabili,” alisema Makamba.
Akiwa mkoani Tabora, Profesa Mark Mwandosya
aliyeambatana na mkewe na mwanaye wa kwanza, alisema hana mbwembwe na si
msanii na ndiyo maana ametaka adhaminiwe na wanachama 30 tu.
Alisema kama kuna mtu anawaeleza kuwa amedhaminiwa
na maelfu ya wanachama siyo mkweli, kwani wanaotakiwa kwa kila mgombea
ni 450 kwa nchi nzima.
Alisema endapo atachaguliwa kuwa mgombea na baadaye kuchaguliwa
kuwa Rais, ataisaidia Tabora katika baadhi ya mambo ikiwemo elimu,
miundombinu na mazingira.
Alisema viongozi wengi walipitia Tabora ambayo ni
sehemu ya vuguvugu la siasa nchini na kama kuna wanaogombea urais na
hawafiki Tabora watakuwa hawafanyi vizuri.
“Nikifanikiwa kuwa Rais nitaufanya mkoa kurudi
enzi zake za kuwa kitovu cha elimu nchini na hili linawezekana
kabisa,”alisema. Alisema akiwa Rais ataufanya mkoa kuwa kiini cha uchumi
kwa kujengwa miundombinu , hasa reli.
Wanachama walalamikia fomu
Idadi ya wanachama waliojitokeza kumdhamini
Profesa Sospeter Muhongo ilizua kasheshe baada ya baadhi yao kukosa
nafasi kwenye fomu zilizotolewa.
Profesa huyo aliyehitimisha ziara yake ya mikoa 15
mkoani Mara alikoanzia, alipata wadhamini 45, lakini wengine walidai
fomu ziliwanyima uhuru wa ‘kujimwaga’ kumdhamini, hivyo kulazimika
kurudi na kadi zao.
Baadhi ya watu waliomdhamini walisema nafasi yake
ya uwaziri wa Nishati na Madini ilikuwa ya uhakika, kwani walikuwa na
uhakika wa kupata umeme vijijini.
Nyalandu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu
akiwa mkoani Mara amewataka wagombea wenzake kuhakikisha wanawasaidia
vijana ili waweze kuinuka kiuchumi na watende haki, kuimarisha umoja
amani na upendo uliopo nchini.
Nyalandu alipata wadhamini 45 na kama ilivyokuwa
kwa Profesa Muhongo baadhi ya wadhamini hawakuweza kujiandikisha
kutokana na nafasi zilizopo kwenye fomu.
Mwigulu Nchemba
CCM Manispaa ya Iringa imempongeza Mwigulu Nchemba
kwa kujiuzulu nafasi ya unaibu katibu mkuu wa chama hicho kwa upande wa
Bara kikisema ni demokrasia ya kweli.
Credit:mwananchi
Akitoa shukrani baada ya Nchemba kuongea na wadhamini, katibu wa
Umoja wa Vijana (UVCCM), Manispaa ya Iringa, Elisha Mwampashi alisema
kitendo hicho kinaonesha ukomavu na utendaji haki ndani ya CCM.
“Tunakupongeza kwa uamuzi wa kuachia nafasi ili
haki itendeke kwenye mchakato wa uteuzi wa nafasi anayoiwania kuteuliwa
na CCM, huu ni mfano wa kuigwa na wengine,” alisema Mwampashi.
Nchemba alisema endapo atachaguliwa kuwa rais atawavusha Watanzania kwa kuifanya nchi kuwa ya kipato cha kati.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha
keki ya Taifa inawafaidisha Watanzania wote kwa kuboresha miundombinu ya
pande zote, sio eneo moja linabadili lami mara tatu wakati jingine hata
mara moja bado.
Katibu wa CCM Manispaa ya Iringa, Zongo Lobe Zongo alisema Nchema alikuwa ametoa maagizo kuwa anahitaji wadhamini 45 tu.
Credit:mwananchi