Kamati ya utendaji ya Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imemfukuza kazi kocha mkuu wa timu ya
Taifa ‘Taifa Stars’ Mart Nooij pamoja na benchi zima la ufundi la Stars
baada ya kipigo cha goli 3-0 kutoka kwa Uganda kwenye mchezo wa kutafuta
nafasi ya kucheza michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi
za ndani (CHAN) mchezo
uliopigwa kwenye uwanja wa Amaan visiwani
Zanzibar.
Kufuatia kutimuliwa kwa kocha na
benchi zima la ufundi la Stars, kitu pekee kinachotakiwa kufanyika ni
kumkabidhi kocha mzawa majukumu ya kukinoa kikosi hicho ambacho kwa sasa
kimepoteza mwelekeo kutokana na vipigo vya mfululizo
Charles Boniface Mkwasa ni kocha
ambaye anauwezo wa kuichukua timu ya Taifa kwa kipindi hiki cha mpito
ambacho tunafikiri nini cha kufanya juu ya haya yote ambayo yametokea.
Licha ya makocha wengi hapa nchini kuwa na leseni za ukocha za daraja A,
Mkwasa ni kocha ambaye yupo kwenye kazi hiyo kwa muda mrefu akifanya
kazi tofauti na makocha wengine ambao wana leseni kama yake lakini
wameziweka ndani bila ya kuzifanyia kazi.
Mkwasa ambye kwasasa ni kocha
msaidizi wa Yanga chini ya Mholanzi Hans van Pluijm, anauelewa mkubwa wa
wachezaji wa Tanzania kuanzia namna ya uchezaji wao na mazingira halisi
ya soka la bongo kwa mapana yake. Amesha kutana nao kwenye timu
mbalimbali wakati timu yake ilipocheza dhidi ya timu hizo kwenye mechi
za ligi akiwa kama kocha.
Lakini tunatakiwa tuelewe kwamba,
Mkwasa siyo nabii hivyo hawezi kuyabadili haya yanayotokea hii leo kwa
siku moja. Anahitaji muda wa kutosha na ushirikiano mkubwa kutoka TFF na
wadau wengine wa soka ili kuweza kupata kile ambacho watu wengi
wamekuwa wakikitamani lakini mwisho wa yote wamekuwa wakiishia kwenye
maumivu.
Tumekuwa na makocha wengi wa
kigeni ‘wazungu’ lakini bado hatujafika popote wala hata nusu ya pale
tunapopataka, nikisema hivyo sina maana nawabeza makocha wa kigeni
waliowahi kuinoa Stars. Ila naangalia kama walifikia malengo ambayo
tumekuwa tukitaka kuyaona kwenye soka letu la Tanzania, kama nao
wamekuwa wanakuja wanalipwa mamilioni ya fedha lakini bado wameshindwa
kutupeleka pale tunapopataka basi sioni ulazima wa wao kuja.
Kumwamini kocha mzawa na kumpa
timu sio dhambi wala si ujinga, kama atapata ushirikiano wa kutosha kama
wanaopewa makocha wa kizungu naamini mzawa anaweza akatusaidia kuliko
hata hawa makocha wa kigeni ambao kila kukicha wanaichukua timu hakuna
wanachokifanya mwisho wa siku tunaishia kuwatimu na kuwalipa pesa nyingi
wanatokomea na kuiacha timu ikiwa kwenye hali mbaya.
Mwarobaini wa taizo letu sio
makocha wa kigeni hapo naomba tuelewane, hata kama tutamchukua Sir Alex
Ferguson, Jose Mourinho, au Pep Guadiola bado tatizo litabaki palepale
kwasababu tatizo letu sisi sio kocha. Tatizo linalolitafuna soka la
Tanzania ni mfumo wazungu wao wanaita ‘system’, hapa ndipo imelala
mizizi ya matatizo yote yanayolitafuna soka la bongo.
Sasa inabidi kuichimbua mizizi
hiyo ili siku moja na sisi tufurahie matunda ya soka kama nchi nyingine
ndogo za Afrika ambazo zimethubutu lakini sisi kila kukicha bado
tunapiga mark time palepale. Mfano mzuri ni Botswana hawa jamaa
waliopata umaarufu kwa ngoma ya ‘makhirikhiri’ walishiriki michuano ya
AFCON sisi tukiwa watazamaji kwenye TV zetu. Nchi nyingine ni Burkina
Faso wale ambao Erasto Nyoni aliwafunga goli wakiwa kwao baada ya kutoka
sare ya 1-1 jijini Dar es Salaam, nao pia walifuzu kucheza AFCON sisi
tukawa watazamaji tu.
Sasa ifike wakati tujifunze
kukubali vyetu, hebu tumpe huyu mzalendo hii timu wakati sisi
tukiangalia tunaanzia wapi kuichimba hii mizizi yetu ya mfumo mbovu
ambao unalitesa na kuligaragza soka letu kila kukicha. Ninaposema timu
apewe Mkwasa sio kwamba nampigia debe la hasha, ila ukiangalia kwa
makocha wazalendo waliopo hapa Tanzania wenye leseni kama ya Mkwasa na
wanafanya kazi basi utaungana na mimi kuomba timu hii apewe Mkwasa mbali
ya kuwa na leseni ya daraja la juu.
Mfano mzuri ni yule kocha wa timu
ya wanawake ‘Twiga Stars’ Rogasian Kaijage, ameweza kuivusha na
kuipeleka kwenye michuano ya All Africa Game itakayopigwa Congo
Brazzaville. Angalia mazingira anayofanyia kazi, wachezaji alionao na
ushirikiano anaopewa kwenye ile timu hapo utajua kuwa hata hawa
wazalendo wanajua ila basi sisi tuna kasumba ya kuwadharau na kutukuza
hao makocha tunaowaamini kuwa watatufikisha tunapotaka.
Kwasasa Stars ipo kwenye wakati
mgumu sana hasa wachezaji wake wanaokipiga kwenye timu hiyo,
wameshapoteza mechi tano mfululizo na hiyo inawaondolea hali ya
kujiamini pindi wawapo uwanjani. Wakishatanguliwa kufungwa wanakata
tamaa wakijua yaliyowakuta kwenye mchezo uliopita yanajiudia tena kwenye
mchezo ambao wanacheza kwa wakati huo. Ukijumlisha na mashabiki wao
kuwazomea hapo ndio mambo yanakuwa magumu kwao kwani wanakuwa wanacheza
kwa presha ya kutaka kuwaridhisha mashabiki.
Endapo tutampa timu Mkwasa, basi
tumuache afanye kile ambacho anaona ni sawa kwa yeye kukifanya kwa
wakati huo. Tusimpe presha kubwa bali tumuamini, tumpe ushirikiano na
kuheshimu yale yote atakayokuwa akiyafanya kwenye kikosi hicho akiamini
yataleta mafanikio. Kweli tupo kwenye wakati mgumu lakini tunatakiwa
kuwa wavumilivu kwenye hili hasa kwa kipindi hiki cha mpito tulichopo
wakati huu.